Muhtasari

Bongoland ni hadithi ya kijana anayeitwa Juma Pondamali. Kijana huyu alikuja majuu akitafuta maisha bora. Kama wengi wetu tunavyoaamini, maisha ya majuu ni maisha bora. Bwana Juma alikuwa na kazi yake nzuri kule Bongoland. Baada ya kumaliza shule form six, alijipatia kazi nzuri sana katika Benki kuu. Baada ya kufanya kazi kwa kama miaka mitatu, akaanza kusuka mipango ya kwenda majuu. Kwa bahati nzuri akafanikiwa na akaondoka kwenda majuu.

Kufika majuu maisha yakawa kama alivyosikia katika miezi ya kwanza. Akapata kazi, akanunua gari hata akapata na msichana wa kimarekani. Mambo yakawa safi. Baada ya muda kidogo, mambo yakaanza kubadilika. Juma akajitahidi kujaribu kumaliza matatizo hayo. Lakini matatizo yakazidi kuwa mengi. Madeni yakaanza kuja, kazi yake ikapunguzwa na mengine mengi. Juma akaendelea kupigana na hali mbaya ya maisha akiwa majuu. Hii ikawa kinyume cha alivyofikiria na alivyosikia kuwa maisha ya majuu ni mazuri sana.

Juma alikuwa na marafiki zake waliojaribu kumsaidia na kumwonyesha jinsi ya kuishi vizuri pale ugenini. Hapo ndipo Juma alianza kuwauliza rafiki zake swali moja la maana sana. "Je ni lipi rahisi, kuwa mtumwa aliyeshiba, au kuwa mtu mwenye njaa aliye huru". Juma aliyaona maisha ya majuu kuwa kama utumwa wa aina fulani. Akaanza kujiuliza kwa nini anaumia hivi. Hasa hasa baada ya kila mtu kumwambia kuwa maisha haya yatakuwa mazuri, kumbe Juma anaona vingine.

Marafiki zake wanaomwambia kuwa maisha ni mazuri hapa kulinganisha na maisha ya Bongoland. Yeye anawauliza kama ni maisha mazuri kwa nini wanalipwa fedha ambazo hazilingani ka kisomo chao. Au kwa nini hawapewi vyeo makazini kwao. Au kwa nini inabidi wafanye kazi zaidi ya moja ili kuishi katika vyumba ya kupanga. Marafiki zake Juma wanaufahamu ukweli lakini wanajaribu na kudai kuwa Juma ana kiwewe. Mtu alitaka kuja majuu, sasa amefika hapa analilia kurudi nyumbani. Hapo hawamwelewi. Wanadai yeye ni kama lele mama. Wanamsihi awe mwanamme na asimame na kuvumilia shida kama wao.

Sinema hii inatafundisha kujiuliza maswali ya Juma kwa wale wenye mipango ya kwenda majuu. Je maisha ni rahisi kuumia mradi uko majuu?. Je angekuwa nyumbani angeyapata matatizo kama hayo? Je atafanya nini kuhusu matatizo haya. Je kwa nini watu walio majuu wanakubali kuishi na matatizo kama haya. Juma, anatusaidia kuelewa na kujaribu kujibu maswali haya.

Unaombwa kuangalia Bongoland na kujiuliza wewe mwenyewe kama ungekuwa Juma ungefanyaje. Ujiulize kama ungechukua hatua kama Juma alizochukua.